Mwanafunzi wa Shahada ya Kompyuta Sayansi (Computer Science) kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Wandowa Titus, amebuni mfumo wa kiteknolojia unaotumia Akili Mnemba (AI) kuhesabu idadi ya abiria katika vituo vya mabasi yaendayo haraka (Mwendokasi).
Akiwa katika maonesho ya wahandisi vijana jijini Dar es Salaam, Titus amesema mfumo huo umetengenezwa mahsusi kusaidia kutatua changamoto ya msongamano mkubwa wa abiria kwenye vituo vya Mwendokasi na kuwezesha usimamizi bora wa usafiri huo wa umma.
Amesema mfumo huo utakuwa na kamera maalumu zitakazowekwa kwenye vituo vya kusubiri mabasi, ambapo zitahesabu idadi ya watu waliopo na kueleza wanaoelekea maeneo tofauti kama vile Kimara, Mbezi, Gerezani na Morocco.
“Hii itawasaidia wasimamizi kujua abiria wangapi wanahitaji huduma kwa wakati fulani na kupeleka mabasi kwa haraka,” amesema Titus.
Ameeleza kuwa wazo hilo lilimjia kutokana na hali ya msongamano mkubwa katika vituo, hali ambayo husababisha kero mbalimbali ikiwemo ucheleweshaji wa huduma na vitendo vya wizi.
“Niliona kuna ulazima wa kuja na suluhu itakayosaidia kupunguza usumbufu kwa abiria na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mabasi ya Mwendokasi,” amesema Wandowa.
Kwa mujibu wake, mfumo huo ukipewa nafasi ya kuendelezwa na kuungwa mkono na mamlaka husika, unaweza kuboresha huduma ya usafiri wa umma jijini Dar es Salaam na kuondoa malalamiko ya abiria kuhusu ucheleweshaji na msongamano kwenye vituo.
Chanzo; Bongo 5