Benki ya NMB imetangaza gawio la kihistoria kwa wanahisa la shilingi bilioni 214.43 na kufikia jumla ya gawio la mwaka la shilingi Bilioni 214.43 kwa wanahisa wake kwa mwaka wa fedha ulioishia Desemba 31, 2024. Pendekezo na uamuzi huo ulipitishwa wakati wa Mkutano Mkuu wa 25 wa wanahisa na malipo ya gawio hili yanatarajiwa kufanyika tarehe 19 Juni 2025 au muda mfupi baada ya hapo, ukiwa ni Mwaka mwingine wa kuwahakikishia wanahisa thamani endelevu. Malipo ya gawio la shilingi bilioni 214.43 ni ongezeko la asilimia 19 ukilinganisha na malipo ya gawio lililolipwa Mwaka 2023 la shilingi bilioni 180.59
Mwaka 2024, Benki ya NMB iliendelea na mwendo mzuri wa utendaji ambapo Benki ilipata faida baada ya kodi ya shilingi bilioni 643 likiwa ni ongezeko la asilimia 19 ukilinganisha na mwaka uliopita. Utendaji mzuri wa benki uliimarisha nafasi yake ya kuendelea kuwa kiongozi na kama mmoja wa Benki zinazofanya vizuri zaidi Afrika Mashariki , na kiongozi wa kweli wa huduma za kifedha.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya NMB Bwana David Nchimbi alisema “Malipo haya ya gawio yanatoa ishara thabiti ya maendeleo na ufanisi wa utekelezaji wa mkakati wetu, misingi imara ya utawala bora, na imani kubwa waliyonayo wanahisa wetu katika mipango yetu ya siku zijazo. Tunaendelea kujikita kwa ari katika kufungua fursa mpya za kimkakati za ukuaji wa huduma za kifedha, kuboresha na kuimarisha huduma kwa wateja wetu, na kujenga ushirikiano wa kudumu wenye tija kwa pande zote. Lengo letu ni kufanikisha maono makubwa ya kuwa mshirika sahihi wa masuluhisho ya kifedha yanayotoa thamani kwa wateja, wawekezaji, na wadau wote kwa ujumla, kwa kuzingatia ufanisi, uvumbuzi, na uwajibikaji wa hali ya juu.”
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi Ruth Zaipuna alieleza yafuatayo “Mwaka 2024 ulikuwa ni mwaka wa kipekee kwa Benki ya NMB , ulioshuhudia maendeleo makubwa dhidi ya mkakati wetu, na kuongeza thamani kwa wadau wetu wote, ufanisi wa kiutendaji na malipo ya gawio hili kubwa kama ilivyopitishwa na wanahisa kunadhibitisha dhamira yetu ya kuwa na ukuaji madhubuti wenye matokeo endelevu.”