Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

NMB Yaendeleza Mkakati wa Kujenga Kizazi Kipya cha Wataalamu wa Fedha

Benki ya NMB Bank Plc imeendelea kuimarisha jitihada za kukuza rasilimali watu wenye ujuzi na maarifa ya kisasa katika sekta ya fedha nchini kwa kudhamini mafunzo maalum kwa vijana 100 kupitia mpango wa Graduate Banker Readiness Programme (GBRP) unaotekelezwa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kupitia ushirikiano huo wa kimkakati, washiriki hupatiwa mafunzo ya kitaaluma yanayochanganya nadharia na vitendo, yakilenga kuwapa uelewa mpana wa shughuli za benki na sekta ya fedha kwa ujumla. Kundi la nne la washiriki limehitimu mafunzo hayo Ijumaa iliyopita, likijiunga na makundi yaliyotangulia kunufaika na programu hiyo.

Akizungumza kabla ya kukabidhi vyeti kwa wahitimu, Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu wa NMB, Bi. Erica Hanson, alisema kuwa mpango huo umebuniwa mahsusi kuziba pengo kati ya elimu ya darasani na uhalisia wa kazi katika taasisi za kifedha.

Alieleza kuwa washiriki wamejengewa uwezo katika maeneo muhimu ikiwemo uchambuzi wa kifedha, uendeshaji wa benki, usimamizi wa vihatarishi, uzingatiaji wa kanuni, utoaji bora wa huduma kwa wateja pamoja na matumizi ya mifumo ya benki ya kidijitali.

“Mahafali ya vijana hawa yanaimarisha zaidi dhamira ya NMB ya kuendelea kuwa mwajiri kinara nchini, jambo lililothibitishwa na kutunukiwa Tuzo ya Mwajiri Bora kwa miaka mitatu mfululizo. Hii ni matokeo ya uwekezaji wa makusudi katika maendeleo ya watu na vipaji,” alisema Bi. Hanson.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitivo cha Biashara wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Omari Mbura, alisema mpango huo unachangia kupunguza pengo la ujuzi katika soko la ajira kwa kuhakikisha wahitimu wanakuwa tayari kukidhi mahitaji halisi ya tasnia ya fedha.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Mratibu wa mafunzo kutoka Kituo cha Utafiti wa Benki na Huduma za Kifedha (CBFSR), Prof. Esther Ishengoma, pamoja na Mkuu wa Idara ya Fedha, Dkt. Thobias Swai, waliobainisha kuwa ushirikiano kati ya sekta binafsi na vyuo vikuu ni nguzo muhimu katika kuandaa wataalamu bora wa baadaye.

Akizungumza kwa niaba ya wahitimu, Marcelina Evarist aliishukuru NMB kwa kuanzisha na kufadhili mpango huo, akisema umewapa ujuzi, kujiamini na uelewa mpana wa sekta ya fedha, hatua itakayowawezesha kushindana katika soko la ajira.

Kuhusiana na mada hii: