Katika tukio la kushangaza linaloonyesha kwa uhalisia madhara ya migogoro ya muda mrefu mfanyabiashara wa simu jijini Tripoli nchini Libya hatimaye amepokea mzigo wa simu januari mwaka huu aliouagiza mwaka 2010 ikiwa imepita miaka 16 tangu aagize mzigo huo.
Mzigo huo ulizuiliwa kwa muda mrefu kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza 2011, kuvunjika kwa miundombinu, kushindwa kwa mifumo ya forodha pamoja na kutokuwepo hali ya usalama nchini humo.
Simu hizo ni za zamani zenye vitufe, zikiwemo Nokia za “Music Edition” na Nokia Communicator ambazo wakati huo zilikuwa alama ya hadhi ya juu, lakini sasa kutokana na ukuaji wa teknolojia tayari zimepitwa na wakati.
Baada ya kusahaulika kwenye maghala kwa zaidi ya muongo mmoja, hatimaye zilifika dukani, jambo lililomfanya muuzaji ashindwe kujizuia kucheka alipokuwa akifungua boksi na kujiuliza kama ni simu au ni vielelezo vya kihistoria.
Video ya tukio hilo ilisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, ikiwachekesha wengi huku ikichochea mjadala mpana kuhusu jinsi migogoro inavyoweza kuvuruga maisha ya kawaida na biashara, cha kushangaza zaidi, mzigo huo ulitumwa na kupokelewa ndani ya jiji moja la Tripoli, umbali wa kilomita chache tu lakini ukachukua miaka 16 kufika.
Chanzo; Millard Ayo