Ni mwaka wa sita sasa, Soko Kuu la Job Ndugai la jijini Dodoma bado halina watu, lakini waliopo wameendelea kupungua kila kukicha huku mitaa na barabara za ndani ya jiji zikifurika wafanyabiashara ndogondogo (machinga).
Hata hivyo, uongozi wa jiji unasema hawatatumia nguvu kupeleka wafanyabiashara huko, badala yake wanaboresha miundombinu ambayo itavuta kundi la watu ambao watakuwa ndiyo wateja wakubwa kwa wafanyabiashara.
Soko la Ndugai ambalo kabla lilijulikana kama Soko Kuu la Dodoma, limejengwa katika Kata ya Nzuguni na ujenzi wake uligharimu zaidi ya Sh14 bilioni ambapo lilianza kufanya kazi rasmi mapema mwaka 2020 likitaraji kuchukua idadi kubwa ya wafanyabiashara.
Hata hivyo, hali imekuwa ni kinyume na matarajio kwani wafanyabiashara wengi waliochukua vizimba na fremu za maduka walikimbia siku chache baadaye kwa kilichoelezwa kuwa hakuna wateja kwani limejengwa nje ya mji.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara katika soko hilo, Maulidi Ally, amesema hali ya biashara kwa sasa ni ngumu kwani wanaofanya biashara hapo wamepoteza mitaji yao na kujikuta wanakuwa na madeni kila mahali huku uendeshaji wa familia zao ukiwa mgumu.
Akizungumzia soko hilo, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dk Frederick Sagamiko, amekiri kuwa soko hilo ni tupu lakini amesema ni muda mfupi watu watakimbilia huko wenyewe na hakutakuwa na nafasi ya kupata kwa urahisi kama wengi wanavyodhani.
Chanzo; Mwananchi