Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

Kunenge Ailekeza TRA Iweke Utaratibu Mzuri Ulipaji Kodi Bila Shuruti

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ameielekeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Pwani kuhakikisha inaweka utaratibu mzuri wa ulipaji kodi ambao utamwezesha kila mmoja kutimiza wajibu huo bila ya shuruti.

Kunenge alitoa wito huo Septemba 24, wakati akizindua Dawati Maalumu la Uwezeshaji Biashara kwa Mkoa wa Pwani, katika hafla iliyofanyika mjini Kibaha.

Amesema uanzishwaji wa dawati hilo ni hatua muhimu kwa sababu utarahisisha utatuzi wa changamoto zinazowakabili wafanyabiashara, lakini amesisitiza kuwa ni lazima TRA iendelee kujenga mazingira rafiki kwa walipa kodi.

Vilevile, Kunenge ameipongeza TRA Mkoa wa Pwani kwa kuendelea kuvuka malengo ya makusanyo kila mwaka, akieleza kuwa jitihada hizo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais kuhusu kuongeza makusanyo ya mapato ya serikali.

Ameongeza kuwa Mkoa wa Pwani unaendelea kushuhudia ongezeko la uwekezaji katika sekta ya viwanda, ambapo mwaka 2021 vilikuwa viwanda 1,387 na hadi sasa vimefikia 1,631.

Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani, Masawa Masatu, amesema kuanzishwa kwa dawati hilo ni utekelezaji wa maelekezo ya serikali katika kushughulikia changamoto za kodi na zisizo za kodi. Amesisitiza kuwa dawati hilo linalenga kuimarisha ushirikiano kati ya mamlaka hiyo na wafanyabiashara pamoja na kuwaunganisha na wadau wengine.

Aidha, Katibu Tawala Msaidizi wa Sekta ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji mkoani humo, Ritta Magere, amesema dawati hilo litakuwa chachu ya kutatua changamoto za wafanyabiashara na kuchochea maendeleo ya uchumi wa mkoa.

Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Wafanyabiashara Wadogo (Machinga), Philemon Maliga, ameahidi kuwa machinga wataendelea kuunga mkono juhudi za kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa.

 

Chanzo; Nipashe

 

Kuhusiana na mada hii: