Mpango wa kuendeleza sekta ya Uvuvi wa Mwaka 2021/22-2036/37 unaendelea kutekelezwa na serikali ikiwamo kufufua viwanda vya kuchakata samaki.
Hatua hiyo inalenga kuendeleza, kuanzisha, kuimarisha na kufufua viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi nchini ili kufikia kwenye uchumi wa viwanda unaoongozwa na sekta binafsi kwa maendeleo ya watu.
Hayo ameyasema Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Ng’wasi Kamani wakati akijibu swali la Mbunge wa Nyamagana (CCM) John Nzilanyingi.
Mbunge huyo alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kushirikiana na sekta binafsi kufufua viwanda vya kuchakata samaki ili kuongeza ajira na mapato.
“Ili kuhakikisha viwanda vyetu vinafanya kazi kulingana na matarajio ya serikali, wizara ipo katika hatua za maamuzi kulingana na taratibu za serikali kuanzisha mamlaka ya uvuvi kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa rasilimali za uvuvi na kupambana na uvuvi haramu.
"Kwa hatua za awali wizara imeweka maboya 32 yenye thamani ya Sh.milioni 224 kwa ajili ya kulinda mazalia ya samaki katika eneo la Luchelele Ziwa Viktoria,” amesema.
Chanzo; Nipashe