Jumla ya vibanda 72 vinavyozunguka Soko la Ichenjezya, wilayani Mbozi mkoani Songwe, vimefungwa na maafisa mapato wa Halmashauri kufuatia mgogoro wa malimbikizo ya kodi ya pango yanayodaiwa kutolipwa tangu mwaka 2021.
Hatua hiyo imesababisha wafanyabiashara 167 wanaofanyia biashara ndani ya soko hilo, wengi wao wakiwa wauzaji wa mbogamboga na matunda, kugoma kwa kufunga biashara zao wakishinikiza wenzao kufunguliwa, wakidai kufungwa kwa vibanda hivyo kunaathiri mzunguko mzima wa biashara.
Mwenyekiti wa Soko la Ichenjezya, Bernad Kabuje, amesema tangu mwaka 2021 hakukuwa na utaratibu rasmi wa ukusanyaji kodi, huku akidai wafanyabiashara hawajawahi kupewa mikataba wala namba rasmi za malipo kutoka Halmashauri.
Ameongeza kuwa tayari suala hilo wamelifikisha kwa Mkuu wa Wilaya, lakini majibu waliyopewa ni kutakiwa kulipa madeni yanayodaiwa ili vibanda vifunguliwe, jambo walilodai halijatoa suluhu ya kudumu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Hamad Mbega, amesema kufungwa kwa vibanda hivyo ni sehemu ya operesheni ya kukusanya madeni ya muda mrefu, huku akibainisha kwamba baadhi ya wafanyabiashara waliingia makubaliano binafsi na kulipa Sh70,000 kwa mwezi badala ya kufanya mikataba halali na Halmashauri inayotoza Shilingi 10,000 kwa mwezi.
Chanzo; Nipashe