Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini zitakazotumika kuanzia leo Jumatano January 07, 2026 saa 6:01 usiku ambapo kwa mwezi huu bei za rejareja za mafuta katika Mkoa wa Dar es Salaam petrol ni Tsh. 2778 kwa lita, dizeli Tsh. 2726 na mafuta ya taa 2763.
EWURA imesema bei za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini zinazingatia gharama za mafuta yaliyosafishwa (FOB) katika soko la nchi za Kiarabu, katika bei kikomo kwa Januari 2026, bei za mafuta katika soko la dunia zimepungua kwa asilimia 4.26 kwa mafuta ya petroli, asilimia 12.83 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 10.44 kwa mafuta ya taa.
Kwa mwezi Januari 2026, gharama za kuagiza mafuta (premiums) katika Bandari ya Dar es Salaam zimepungua kwa wastani wa asilimia 1.1 kwa mafuta ya petroli, asilimia 4.0 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 3.7 kwa mafuta ya taa, katika bandari ya Tanga zimeongezeka kwa asilimia 3.5 kwa petroli na dizeli; na katika bandari ya Mtwara zimeongezeka kwa asilimia 11.5 kwa mafuta ya petroli na hakuna mabadiriko kwenye mafuta ya dizeli.
“Gharama za mafuta (FOB) na gharama za uagizaji (Premiums) zinalipwa kwa kutumia fedha za kigeni ikiwemo Dola ya Marekani, kwa bei za mwezi Januari 2026, wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni (Applicable Exchange Rate) umeongezeka kwa asilimia 1.31, Wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa rejareja wanatakiwa kuuza mafuta kwa bei zinazooneshwa katika Jedwali Na. 3. Aidha, wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa jumla wanatakiwa kuuza mafuta kwa bei zinazooneshwa katika Jedwali Na. 2. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mfanyabiashara yeyote atakayekiuka AGIZO hili”
Itakumbukwa bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini kwa mwezi uliopita zilizoanza kutumika kuanzia Jumatano December 03, 2025 saa 6:01, bei za rejareja za mafuta katika Mkoa wa Dar es salaam petrol ilikuwa ni Tsh. 2749 kwa lita, dizeli Tsh. 2779 na mafuta ya taa 2653.
Chanzo; Millard Ayo