Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Kodi za Ndani (IDRAS) umeelezwa utamwezesha mlipa kodi kujisajili na kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) moja kwa moja bila kulazimika kufika katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Hali hiyo ni tofauti na ilivyokuwa awali ambapo huduma hiyo ilihitaji mhusika kufika ofisini.
Hayo yamesemwa leo Februari 04 na Ofisa Msimamizi wa Kodi wa TRA kutoka Mkoa wa Kikodi Kahama, Jaliwa Wilson, alipokuwa akitoa elimu ya kodi kwa wafanyabiashara pamoja na wasimamizi wa kampuni kuhusu mfumo huo uliokuja na maboresho mbalimbali.
Amesema mfumo huo umeondoa changamoto iliyokuwapo awali ya kubadilisha namba ya simu, ambapo mlipa kodi alilazimika kufika ofisini na kuandika barua ya maelezo kuhusu upotevu wa namba hiyo.
Wilson amesema mfumo huo unamwezesha mlipa kodi kujipatia huduma takribani 15 kwa njia ya mtandao bila kufika ofisini na endapo mlipa kodi atapoteza simu au akahitaji kubadilisha namba ya simu aliyosajili TRA, atalazimika kujibu maswali 11 ndani ya mfumo huo, ili kuthibitisha uhalali wake.
Chanzo; Nipashe