Search

Saved articles

You have not yet added any article to your bookmarks!

Browse articles

GDPR Compliance

We use cookies to ensure you get the best experience on our website. By continuing to use our site, you accept our use of cookies, Privacy Policy, and Terms of Service.

Biashara ya Uji Ilivyobadili Maisha ya Victoria

Biashara ndogo ya kuuza uji imebadilisha maisha ya Victoria Mwelelwa, ambaye sasa ana uwezo wa kulea familia yake, kulipia bili mbalimbali na kuwa na uhakika wa mlo, hali ambayo haikuwa hivyo awali.

Akizungumza na Nipashe Digital, Victoria amesema hapo awali alikuwa akifanya kazi katika genge la mtu mmoja kwa muda mrefu bila kuona maendeleo yoyote. Hali hiyo ilimfanya kufikia uamuzi mgumu wa kuacha kazi Desemba 31 mwaka jana na kubaki nyumbani kama mama wa nyumbani.

Anasimulia kuwa baada ya kukaa nyumbani akiwa na mtoto wake, maisha yalizidi kuwa magumu kiasi cha kumlazimu kumuomba mume wake mtaji. Mumewe alimpatia shilingi 50,000, fedha zilizokuwa mwanzo wa safari yake ya kuingia mtaani kufanya biashara ya kuuza uji.

“Namshukuru Mungu mwanzo wangu haukuwa mbaya. Kila ninapotoka kuuza uji, ninaingiza kitu tofauti na kukaa nyumbani bila kipato. Leo ni siku ya tisa tangu nianze biashara hii. Nikitoka, baada ya kutoa gharama zote ikiwemo kununua Blueband kwa ajili ya wateja wangu, nabaki na shilingi 4,000 ambazo nazitumia kwa matumizi na kuweka akiba,” anaeleza.

Victoria anasema kila siku anafanikiwa kumaliza uji wote anaouza na kupata wateja wengi zaidi. Anaamini kuwa kwa bidii na msaada wa Mungu, ataendelea kukua na hatimaye kufikia mafanikio makubwa zaidi.

“Nimeanza na chupa moja, baadaye nikapata ya pili kwa msaada wa watu walioguswa na hali yangu. Hilo limenifanya niipende zaidi kazi hii. Nawaomba wanawake na vijana wasione aibu kufanya biashara ndogondogo, kwani ndizo zitakazowainua. Mimi leo natembea na mtoto wangu kila mahali, naamini ipo siku tutafanikiwa,” anasisitiza.

Anasema hakutegemea kukutana na watu wenye mioyo ya kusaidia wakati alipoanza kuzunguka mtaani, akiwataja wazee waliompa moyo na kumshika mkono kuwa ni akina Maasa Naftali, Zadocic Munisi (Lowasa) na Elias Ngutunyi, ambao walimpa nguvu ya kuendelea kupambana na biashara yake.

 

 

 

Chanzo; Nipashe

Kuhusiana na mada hii: