Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) amezindua mafunzo ya mfumo mpya wa kidijitali wa Integrated Domestic Revenue Administration System (IDRAS) kwa wadau wa kodi, yanayofanyika kwa muda wa siku tatu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kuzindua mafunzo hayo, Kamishna Mwenda amesema mfumo huo utaondoa malalamiko mengi kutoka kwa wadau na walipakodi, kwa kuwa utawezesha huduma kupatikana saa 24 kwa siku, huku mtumiaji akiwa na uwezo wa kuutumia popote alipo kupitia simu au kifaa kingine cha kielektroniki.
Ameongeza kuwa mfumo wa IDRAS pia utawawezesha wafanyabiashara kutoa risiti za kielektroniki za EFD hata pale ambapo hawana mashine za EFD katika maeneo yao ya biashara.
Kwa mujibu wa Kamishna Mwenda, hatua hiyo inalenga kurahisisha ulipaji wa kodi, kuongeza ufanisi wa mifumo ya ukusanyaji wa mapato na kuboresha mazingira ya biashara nchini.
Chanzo; Global Publishers