Utafiti mpya umeonesha kuwa kunywa kahawa/chai yenye kafeini kila siku ‘kunaweza’ kusaidia kuboresha mzunguko wa damu kwenye ubongo, kupunguza uvimbe wa seli za ubongo na kukulinda dhidi ya baadhi ya mabadiliko yanayohusishwa na kupotea kwa kumbukumbu.
Utafiti uliofanywa kwa Watu zaidi ya laki moja na elfu thelathini Marekani waliokunywa kwa siku vikombe viwili au vitatu vya chai/kahawa yenye kafeini, uligundua kuwa hatari yao ya kupata ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu ilikuwa chini kwa 15% hadi 20, Mwandishi Mkuu wa utafiti huo Dr. Daniel Wang, Profesa msaidizi katika Idara ya lishe Harvard T.H. Chan School of Public Health, Boston ameeleza.
Hata hivyo Wataalamu wanasisitiza kuwa matokeo hayo yanaonesha uhusiano tu (association) na sio uthibitisho wa moja kwa moja kuwa ni tiba ya kuzuia ugonjwa wa dementia na kwamba unywaji wa kupita kiasi unaweza kusababisha madhara mengine ya kiafya kama shinikizo la damu au matatizo ya usingizi.
Kwa upande wake Profesa Jules Griffin wa Chuo Kikuu cha Aberdeen anasema bado njia sahihi za kuushinda ugonjwa huo ni Watu kujiepusha kuvuta sigara, kufanya mazoezi na Watu kupunguza ulaji wa vyakula venye mafuta mengi pamoja na sukari katika milo yao.
Dementia ni hali ya kiafya inayohusiana na kupoteza uwezo wa ubongo kufanya kazi zake za kawaida hasa zinazohusiana na kumbukumbu, ufahamu na ujuzi wa kufikiri mfano Mtu kusahau majina ya Watu au matukio ya siku za karibuni, Mtu kupitia changamoto za kufikiri au kupitia ugumu kufanya maamuzi, Mtu kuwa na mchanganyiko wa hasira za haraka au mabadiliko ya hisia ambapo hayo yanaweza kutokana na magonjwa kama Alzheimer’s disease, ugonjwa wa mishipa ya ubongo (vascular dementia), au matatizo mengine ya ubongo.
Chanzo; Millard Ayo