Huko nchini Latvia, hali isiyo ya kawaida imeibuka kufuatia upungufu mkubwa wa wanaume, jambo lililowalazimu wanawake wengi kuanza kuajiri kile kinachoitwa “waume kwa saa”
Kwa mujibu wa The Business Standard na New York Post takwimu za Eurostat zinaonyesha Latvia ina asilimia 15.5 zaidi ya wanawake kuliko wanaume, mara tatu ya wastani wa Umoja wa Ulaya.
Aidha kwa wenye umri zaidi ya miaka 65, idadi ya wanawake ni mara mbili ya wanaume, kwa mujibu wa World Atlas.
Changamoto hiyo ya uwiano wa kijinsia imeifanya wanawake wa Latvia nchi maarufu kwa misitu ya misonobari, tamaduni za kale na miji yenye mandhari ya kihistoria, kulalamika kukosekana kwa wanaume wa kuchangamsha au hata kufahamiana nao.
Kwa kuliziba pengo hilo, wanawake nchini humo wameanza kutumia huduma maalumu za kukodi wanaume kwa muda mfupi ili kusaidia shughuli za nyumbani na kuwachangamsha.
Sababu zilizotajwa na wataalamu ni kwamba wanaume wanavuta sigara mara tatu zaidi ya wanawake, ambapo ni asilimia 31 ya wanaume dhidi ya asilimia 10 tu ya wanawake.
Asilimia 62 ya wanaume ni wanene au wanene kupita kiasi, ikilinganishwa na asilimia 57 ya wanawake, hivyo sababu hizo zinachangia kupunguza umri wa kuishi kwa wanaume.
Chanzo; Mwananchi