Shirika la Anga la Marekani (NASA) kwa mara ya kwanza kupitia sera mpya inayotegemewa kuanza hivi karibuni, limetangaza kuwaruhusu Wanasayansi wa anga za juu kusafiri na simu janja zao ( smartphones ) ambapo mabadiliko haya yanakuja kabla ya uzinduzi wa safari ya pili ya mpango wa NASA kurudisha Binadamu mwezini ( Artemis 2) inayotarajiwa kupeleka Wanasayansi wanne kwenye safari ya siku 10 kuuzunguka mwezi.
Kwa kipindi kirefu Wanasayansi wa anga za juu wa NASA waliokuwa na shauku za kupiga picha za angani hawakuweza kunasa na kurekodi mazingira na mandhari za kipekee za anga hizo za juu kutokana na kutoruhusiwa kubeba simu zao na badala yake kutumia vifaa vya Shirika hilo ambavyo ni maalum kwa matumizi ya angani.
Swali ambalo wengi watajiuliza ni wataweza kuzitumia simu kupigia familia zao ? jibu ni HAPANA kwasababu huko angani au kwenye mzunguko wa mwezi hakuna mtandao wa kawaida wa simu hivyo watarekodi picha/video na kisha kuzituma duniani kwa njia za satellite kupitia vifaa vya NASA.
Wengine wanaweza kuona hili ni jambo dogo na kuhoji “sasa simu ni za nini kama zitatumika kupiga picha tu ?....... Wataalamu wanasema kwa mazingira ya anga za juu habari hii ni ‘big deal’ kwa sababu kadhaa ikiwemo mazingira ya anga kuwa hatari kwa vifaa vya kawaida kutokana na mionzi mikali na kwamba simu hazikutengenezwa kwa mazingira hayo ilikuwa ni lazima NASA ijihakikishie kuwa hazitosababisha hitilafu ya umeme au kuvuruga mawasiliano ya chombo na pia betri zake haziwezi kuhatarisha usalama.
Chanzo; Millard Ayo